OFFICIAL: UONGOZI SIMBA WAKANUSHA KUWEPO KWA MKUTANO MKUU KESHO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wana
habari,
KUMEKUWAPO
na taarifa za kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Simba uliopangwa
kufanyika Kesho (Machi 17, 2013) jijini Dar es Salaam kujadili mustakabali wa
klabu.
Ikumbukwe
kwamba Mkutano Mkuu wa Wanachama ndiyo chombo cha juu kabisa cha maamuzi kwa
klabu yetu. Katiba ya Simba SC imeupa Mkutano Mkuu hadhi ya juu mno na ndiyo
maana imeweka utaratibu wa kufanyika kwake.
Miongoni
mwa utaratibu ni kwamba ni lazima uitishwe na Mwenyekiti aliye madarakani wa
klabu. Kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji, ndiye atakayepanga ajenda, mahali
na wakati wa kufanyika kwa mkutano wenyewe.
Katika
miaka ya nyuma, zilikuwepo nyakati ambapo klabu ilikaa hadi miaka mitatu pasipo
kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wowote wa wanachama. Hakuna mwanachama au kikundi
chochote kilichojitokeza kudai mkutano wa dharura wakati huo ingawa ilikuwa
ikifahamika kwamba huo ulikuwa ni ukiukwaji mkubwa wa katiba ya
klabu.
Tangu
uongozi huu uingie madarakani takribani miaka mitatu iliyopita, mikutano mikuu
miwili ya wanachama imefanyika kwa mujibu wa KATIBA. Mungu akijaalia, uongozi
huu utafanya mkutano mwingine wa kawaida wa wanachama baadaye mwaka
huu.
Hata
hivyo, kwa kuzingatia hali halisi ya klabu, Mwenyekiti wa Simba, Alhaji Ismail
Aden Rage (Mb), mwezi uliopita alitangaza dhamira yake ya kuitisha Mkutano Mkuu
wa Dharura wakati wowote kuanzia sasa.
Rage
alisema mkutano huo ungekuwa na ajenda moja tu; Kujadili Mwenendo wa Klabu
kwenye mashindano inayoshiriki msimu huu.
Kwa bahati
mbaya, Mwenyekiti alishikwa na maradhi na akapelekwa India kwa matibabu na yuko
huko hadi Mola atakapomjalia afya njema na kurejea. Kuna uwezekano mkubwa,
Inshallah, akarejea mwishoni mwa wiki ijayo.
Hii maana
yake ni kwamba uongozi umeridhia kufanyika kwa Mkutano wa wanachama. Kimsingi,
kama uongozi umeridhia, hakuna mwanachama mwingine anayeweza kuitisha mkutano
mkuu mwingine.
Mwenyekiti
ameruhusiwa kuitisha Mkutano Mkuu kwa sababu alichaguliwa na wanachama na hivyo
ana nguvu ya kisheria (locus standi) kufanya hivyo. Hawa wengine
wanaoitisha mkutano wana nguvu gani ya kisheria kufanya hivyo? Walichaguliwa na
nani kuwakilisha wanachama? Lini na wapi?
Uongozi
pia unaweza kuitisha mkutano kwa vile wenyewe ndiyo wenye leja ya wanachama.
Klabu sasa ina database yake ya kompyuta inayotambua wanachama walio hai na
wasio hai.
Kwa
kutumia database hiyo, uongozi huu unatambua wanachama walio hai na wasio hai.
Hakuna mtu mwingine yeyote, aliye nje ya uongozi huu anayefahamu wanachama walio
hai na wasio hai. Hao wanachama wanaoitana kufanya mkutano, wamehakikiwa na nani
kubaini uhalali wao huo?
Uongozi wa
Simba SC unaona kwamba wale wanaolazimisha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wana
ajenda binafsi na si za maslahi ya klabu. Kama kweli wangekuwa na nia njema na
klabu wangesubiri mkutano ambao utaitishwa punde.
Kwani,
kuna uharaka gani wa kufanyika mkutano kesho? Kwanini hawataki Mwenyekiti,
ambaye wanachama walimpa mamlaka ya kuongoza klabu kwa kipindi cha miaka minne,
awepo kwenye mkutano huo?
Kwanini
hawataki kuungana na wana Simba wengine kumwombea Mwenyekiti kwa Mungu ili
amwepushe na ugonjwa na kumrejesha salama hapa nyumbani? Kwanini mikutano hii
iitishwe katika kipindi ambacho uongozi umefungua mikono yake na kukaribisha
kila mmoja mwenye mapenzi mema na klabu kuja kuchangia?
Kwenye
macho ya Katiba ya Simba na sheria za Tanzania, huu mkutano wa kesho ni batili
na una lengo la kuleta vurugu na mifarakano kwenye jamii na michezo kwa ujumla
wake. Michezo ni amani na furaha na michezo si vurugu.
Tayari
uongozi wa Simba umetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na ubatili wa mkutano huo. Tunapenda kuwaomba
wanachama wetu wasiopenda fujo na vurugu kwenye michezo kukaa mbali na mkutano
huo kwa vile vyombo vya dola vitaufuatilia.
Uongozi
hautajiingiza katika kutoa dhamana au msaada wa namna yoyote kwa yeyote ambaye
atachukuliwa hatua na vyombo vya dola kutokana na kujihusisha na mkutano
huo.
Pia, Simba
SC inatoa wito kwa vyombo vya habari kuwa makini wakati vinaporipoti matukio ya
vurugu kwenye michezo. Kabla mtu hajahojiwa kujieleza kama mwanachama wa Simba,
ni vema kwanza akaonyesha kadi yake ya uanachama na risiti za malipo
yake.
Wakati
mwingine, waandishi huwa tunawapa nafasi kwenye vyombo vyetu vya habari watu
ambao hawana mchango wowote kwenye kukuza michezo bali kuleta vurugu. Kwanini,
tungejiuliza, ni watu wale wale ambao kila mwaka huonekana wakati wa vurugu na
wakati wa amani huwa hawaonekani?
Kwanini,
vyombo vyetu vinatoa nafasi kwa watu ambao lengo lao ni kuhakikisha vilabu vyetu
vinazidi kubaki nyuma, vinakuwa na vurugu kila wakati na michezo inaonekana kama
ni sehemu ya wahuni na watu wasio na utaratibu?
Mpira bado
haujaleta tija kubwa kwenye uchumi wa Tanzania na kunufaisha wachezaji kwa
sababu baadhi ya watu makini na makampuni makubwa yanaogopa kujiingiza kwenye
michezo kwa sababu ya tabia kama hizi.
Ni vema
vyombo vya habari vikafanya jitihada kubwa katika kuwatambua waleta vurugu, si
katika klabu ya Simba pekee, bali kwenye sekta ya michezo kwa ujumla, ili
visiwape nafasi ya kuharibu na badala yake vitoe nafasi kwa wale wenye lengo la
kujenga.
Tunasisitiza, uongozi huu utaitisha
Mkutano Mkuu wa Wanachama Wote mara baada ya kurejea kwa
Mwenyekiti.
Imetolewa
na
Ezekiel
Kamwaga
Ofisa
Habari
Simba
SC
Comments
Post a Comment