Madai kuwa kiwango cha elimu nchini kimeporomoka yametawala katika ndimi za wadau wengi wa elimu. Matokeo mabaya ya mitihani hasa ile ya Taifa imekuwa ikitumika kama hoja mojawapo ya kushadadia hali hiyo.
Upi ukweli kuhusu kiwango cha elimu yetu? Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anaelezea hali halisi ya elimu nchini kama alivyohojiwa na mwandishi wetu.
Swali: Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa kwa Watanzania ni bora?
Jibu: Ili kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa kwa Watanzania ni bora, Serikali imepanga kufanya yafuatayo katika mwaka wa fedha 2013/14: Kwanza, kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote za elimu kwa kuongeza idadi ya walimu na wakufunzi na hasa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati, Teknolojia na Lugha katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari; kutoa mafunzo ya kuongeza ufanisi katika ufundishaji na kujifunza kwa walimu ikiwa pamoja na kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu; kuendesha na kuongeza idadi ya maktaba katika kanda, shule na vyuo kwa lengo la kujenga utamaduni wa kujisomea.
Mengine ni kuongeza wingi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, vikivitabu kwa kushirikiana na wadau wengine hasa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI; kuimarisha ukaguzi wa shule na vyuo, usimamizi na uendeshaji wa elimu na mafunzo pamoja na shughuli za ufuatiliaji na tathmini kwa azma ya kuifanya Idara ya Ukaguzi wa Shule kuwa mamlaka inayojitegemea.
Kuhusu elimu ya juu, Serikali itajenga uwezo wa taasisi za elimu katika kutoa elimu ya juu iliyo bora na inayolingana na mahitaji ya soko. Hilo litatokana na kujenga uwezo wa watendaji wa taasisi za elimu ya juu katika maeneo ya uongozi ili kuimarisha utawala bora; kuendelea kutoa ufadhili wa shahada ya uzamili na uzamivu kwa wahadhiri na wahadhiri wasaidizi na kuendelea kuboresha maslahi ya wahadhiri.
Swali: Pamoja na mikakati hiyo, kuna madai kuwa kiwango cha elimu nchini kimeporomoka, je, ni kweli na nini kimechangia hali hiyo?
Jibu: Kwanza kabisa ingefaa kujiuliza kiwango cha elimu ni nini na kinapimwa vipi au kinapimwa kwa viashiria gani? Pili ingefaa kujiuliza ni lini tunaweza kusema kuwa tulifikia kiwango sawia cha elimu yetu na hivyo kwa sasa tukilinganisha na wakati huo tunaweza kusema kuwa kiwango chetu cha elimu kimeshuka. Na kama kimeshuka kimefika wapi?
Baadhi ya wadau wana dhana kuwa kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa mitihani ya taifa ni kiashiria pekee na tosha cha kushuka kwa kiwango cha elimu. Pia wengine hudhani kuwa kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiingereza ni kiashiria cha kiwango cha juu cha elimu. Hivi sio viashiria pekee vya kiwango cha ubora wa elimu nchini.
Swali: Ni vipi hivyo viashiria vingine?
Jibu: Kiwango cha elimu maana yake ni uwezo wa mtu kutenda na kumudu ushindani katika stadi mbalimbali, kutokana na elimu aliyopata katika mfumo wa elimu husika. Kupanda na kushuka kwa kiwango cha elimu kunaweza kupimwa kwa kulinganisha uwezo wa mtu wa kutenda na kumudu ushindani katika stadi mbalimbali kutokana na elimu aliyoipata kwa kuangalia muda na mahali alipopata elimu hiyo.
Comments
Post a Comment