Inspekta wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Yona Afrika akizugumza na Meneja wa Kiwanda cha nondo cha Metro cha jijini Dar es Salaam, Onesmo Ngondo mara baada ya TBS kukifungia kiwanda hicho kwa muda usiojulikana , kutokana na kuzalisha nondo zisizo na viwango vya ubora vinavyotakiwa. Picha na Beatrice Moses |
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limevifungia viwanda viwili vya kuzalisha nondo kwa muda usiojulikana.
Viwanda vilivyofungiwa ni vya Metro Steel Mills kilichoko Vingunguti Dar es Salaam na Quaim Steel Milis kilichopo Chang’ombe wilayani Temeke.
Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kwamba vimekuwa vikizalisha na kuuza nondo zisizo na ubora wa viwango vinavyokubalika na hivyo kuwa tishio kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Quaim, Hassan Amir, alisema kiwanda chake kilianza kuzalisha nondo tangu mwaka 2006.
Katika maelezo yake, , alipinga hatua hiyo ya TBS akidai kwamba inafanywa kinyume cha sheria, kwa madai kuwa hakupewa barua kabla ya amri ya kukifunga kiwanda chake.
Hata hivyo Mwanasheria wa TBS Baptista Bitao alisisitiza uhalali wa hatua hiyo, akieleza kuwa inafanywa kwa kuzingatia sheria inayompa mamlaka Inspekta wa shirika hilo kukifungia kiwanda kinachokiuka sheria ya viwango ya mwaka 2009.
Comments
Post a Comment