WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, amesema atakuwa tayari kuwania urais mwaka 2015, iwapo wananchi wataona anafaa na kumtaka afanye hivyo.
Alisema
hayo juzi wakati akijibu maswali ya mwandishi wa habari hii mjini Iringa,
baada ya kumalizika kwa kongamano la vyuo vya elimu ya juu mkoani hapa,
lililofanyika katika ukumbi wa St. Dominic.
Membe aliyekuwa mgeni rasmi katika
kongamano hilo, alisema ingawa muda wa kufanya uamuzi kuhusu mwaka 2015
bado na chama hakijatoa utaratibu, lakini atasubiri ushauri wa
Watanzania.
"Naomba kurudia, mimi nilishapata
kuueleza umma kuwa muda bado haujafika wa kutangaza kugombea urais
...ila nasema hivi natarajia sana ushauri wa Watanzania.
“Iwapo
Watanzania wataniona nafaa na kunitaka nigombee, nitapima mawazo yao na
iwapo ni wananchi wengi watakaoniunga mkono kutaka nigombee, basi
nitachukua fomu na kuijaza ili nigombee nafasi hiyo kwani sauti ya wengi
ni sauti ya Mungu," alisema Waziri Membe.
Maadili ya wabunge Membe alisema hali ya
kisiasa nchini inakwenda vibaya kutokana na kila mtu kuzungumza mambo
bila kujitathmini.
Alisema mbaya zaidi hata baadhi ya wabunge wa CCM,
nao wamekuwa si msaada kwa chama, kutokana na kuzungumza mambo dhidi ya
Serikali na chama.
Membe alisema amepata kukaa bungeni kwa
zaidi ya miaka 15 tangu Bunge la Spika Pius Msekwa, hadi sasa chini ya
Spika Anne Makinda, ila anachokiona ni baadhi ya wabunge kukosa maadili
na kuzungumza mambo bila kuzingatia kanuni za Bunge, jambo ambalo ni
hatari zaidi.
Alisema Bunge linalotazamwa na
Watanzania, ni lazima liwe la mfano wa kuigwa na lenye kuzingatia
maadili katika kuzungumza, lakini sasa ndio maana Bunge linaendelea
kupoteza mwelekeo.
"Bunge linapoteza mwelekeo kutokana na mawazo ya
baadhi ya wabunge wanaofikiri wakisema ovyo na kutumia lugha kali katika
kuzungumza, wao ndio wanaonekana ni wabunge bora kitu ambacho hakipo.
“Mbunge ni pamoja na kujiheshimu na kutumia lugha nzuri katika kuwakilisha wapiga kura wako bungeni," alisema.
Membe alisema kutotumia busara katika
kujadili mambo bungeni, si ubunge mzuri na bora watambue wazi kuwa
wananchi wao wanawatazama na hukumu yao itatolewa mwaka 2015 katika
uchaguzi mkuu kama hicho wanachokifanya, ni kuwakilisha wananchi au
kujiwakilisha.
"Nawaomba wabunge wawe wazalendo,
wawakilishe wananchi waliowatuma badala ya kuligeuza Bunge kama sehemu
ya kuonesha ujuzi wa kuzungumza ovyo.
“Nasema tuogope wananchi, mwaka 2015
watatoa adhabu kwa kila mbunge na kwa sasa wananchi wanasikiliza na
kutazama ila muda ukifika watakuacha," alisema.
Alisema wabunge wengi ni vijana na
wanafikiri kusema vibaya juu ya CCM ndio ubunge bora, ila watu watafanya
uchunguzi wa kutembelea jimbo la mbunge husika na kuangalia amefanya
nini katika jimbo lake na watampima kwa kazi aliyofanya na si ukali
bungeni.
Alisifu baadhi ya wabunge wa CCM, kwamba
wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika majimbo yao, kwa chama na
Serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete, kwa kusukuma mbele maendeleo ya
Taifa, ila baadhi yao wapo kwa ajili ya kuonesha uwezo wa kusema ovyo.
Comments
Post a Comment