WAKATI muda unazidi kuyoyoma kuelekea mchezo mkali wa ligi kuu soka Tanzania bara hapa jijini Mbeya baina ya wenyeji wa uwanja wa sokoine, “Wajelajela”, Tanzania Prisons dhidi ya wakali wa mashamba ya miwa ya Manungu Turiani Mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar, kocha wa klabu ya Mtibwa, Mecky Mexime ametoa kali ya mwaka baada ya kuwaponda vikali wanaosema uwanja huu ni mbovu.
Akizungumza jijini hapa, Mexime amesema wanaosema uwanja wa Sokoine na mbaya hawana maana yoyote katika soka la Tanzania, kwani umekaguliwa na TFF na umekubalika, zaidi hata hao wanaosema uwanja haufai, hawana hata wa mazoezi.
“Mbona viwanja vyetu tunavijua sana, hawa wanaosema uwanja huu ni mbovu, mbona wanafanyia mazoezi viwanja vibovu zaidi. Waache siasa katika soka pale wanaposhindwa, wacheze mpira na kuacha visingizio visivyokuwa ba maana”. Alisema Mexime.
Zaidi Mexime amewaacha hoi mashabiki wa soka baada ya kusema kuwa; kama mtu anasema uwanja wa Sokoine mbaya, anataka mpira ukachezwe kwenye magodoro ya vitandani?.
“Kama uwanja huu ni mbaya, sasa wanataka tukachezee kwenye magodoro?”. Alihoji Mexime.
Akizungumzia pambano la leo dhidi ya Tanzania Prisons, Mexime amesema itakuwa mechi nzuri sana na yenye mvuto kwani daima klabu yake inacheza soka la kuvutia.
“Sisi kazi yetu ni kucheza soka, sio kama hao wanaosingizia uwanja kila kukicha, tutapiga soka la ukweli”. Alisema Mexime.
Wakati huo huo nao Tanzania Prisons wamesema wako makini na mechi ya leo, hivyo wamewatoa shaka mashabiki wa Mbeya.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Jumanne Chale amesema wachezaji wake wana morali kubwa ya kusaka ushindi na kwa kiasi kikubwa wanategemea kushinda baada ya kutoa sare jumatano ya wiki hii dhidi ya Yanga.
Wao Mtibwa walitoa suluhu na Mbeya City katika uwanja wao wa Manungu siku ya jumatano.
Comments
Post a Comment