Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ulioituhumu Serikali ya Tanzania.
--------------
Na Fatma Salum-MAELEZO
SERIKALI ya
Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi yake
zilizotolewa na mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ujulikanao kama www.standardmedia.co.ke unaosadikika kuendeshwa na kampuni ya gazeti la The Standard la nchini humo.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene , alisema
mtandao huo umeripoti kuwa Serikali ya Tanzania imekataa kuiuzia Kenya
gesi asili ya Songosongo jambo ambalo halina ukweli kwa kuwa gesi
inayozalishwa hivi sasa bado haijafikia kiasi cha kuweza kuuzwa nje ya
nchi.
Mtandao
huo pia umeripoti kuwa Serikali ya Tanzania ilikataa viwanja vyake vya
ndege vya kimataifa kutumiwa na ndege zilizopaswa kutua katika uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata wakati wa ajali ya moto iliyotokea
kwenye uwanja huo hivi karibuni.
Mwambene
alifafanua kuwa tuhuma hizo ni za uongo kwani mara baada ya uwanja wa
ndege wa Jomo Kenyata kuwaka moto, ndege zilizotakiwa kutua uwanjani
hapo ziliruhusiwa kutua kwenye viwanja vya ndege vya Tanzania vya Julius
Nyerere International Airport (JNIA) na Kilimanjaro International
Airport (KIA).
“Sio
kweli hata kidogo kwamba Tanzania ilikataa ndege za Kenya zisitue
kwenye viwanja vyake kwa sababu uwanja wa Jomo Kenyata ulipoungua ndege
nyingi zilizopaswa kutua katika uwanja ule zilitua kwenye viwanja vyetu
na hii pia ilitokana na ukweli kwamba Tanzania na Kenya zinachangia
ndege nyingi za nje ya nchi.” Alisema Mwambene.
Aidha
Mwambene alikanusha tuhuma nyingine iliyodai kuwa mwaka 2010 Tanzania
ilikataa kuiuzia Kenya chakula badala yake ikaiuzia nchi ya Uganda
taarifa ambazo si za kweli kwa kuwa mwaka huo nchi nyingi za Afrika
zilikumbwa na baa la njaa ikiwemo Tanzania yenyewe.
Hivyo Tanzania ililazimika
kusitisha utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara kuuza chakula nje ya
nchi na hakukuwa na taarifa yoyote ya kuuzwa chakula nchini Uganda.
Kutokana
na upotoshaji huo Mwambene alisema Serikali ya Tanzania imeutaka
mtandao huo kuomba radhi na isipofanya hivyo hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yake.
Katika
hatua nyingine Mwambene alifafanua kuwa zoezi linaloendelea nchini la
kuwataka wahamiaji haramu wanaoishi hapa kinyume cha utaratibu kuondoka
kwa hiari haliwahusu wakimbizi waliopo nchini kisheria.
Pia
zoezi hilo linawalenga wahamiaji haramu wote kutoka nchi za Rwanda,
Burundi, Congo DRC, Zambia na Uganda na hakuna serikali ya nchi yoyote
kati ya hizo iliyolalamika kuhusu hatua hiyo.
“Mpaka
sasa zoezi linaenda vizuri hakuna taarifa yoyote ya malalamiko kutoka
Zambia, DRC, Burundi, Rwanda wala Uganda na tayari Rwanda imetuma
taarifa rasmi kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendesha vema zoezi
hilo.
Kinachoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari ni upotoshaji
unaolenga maslahi binafsi.”
Akizungumzia
usalama wa Watanzania nchini Rwanda, Mwambene alisema hakuna taarifa
ya Mtanzania yeyote kunyanyaswa nchini humo na uhusiano wa
kidiplomasia kati ya Rwanda na Tanzania haujakatika.
Comments
Post a Comment