BARCELONA, HISPANIA
WAKATI Rais wa Barcelona, Sandro Rosell na kocha wa zamani wa timu hiyo, Mdachi Johan Cruyff, wakiwa hawatazamani usoni, suala la usajili wa Mbrazili Ronaldinho, linadaiwa kuwa chanzo kikuu cha uhasama wa wawili hao.
Kwa mujibu wa Rosell, Cruyff alichukia kutokana na kusajiliwa kwa Ronaldinho tofauti na matakwa yake.
Cruyff aliyewahi kuwa kocha wa Barcelona kati ya mwaka 1988 na 1996, amekuwa akirushiana maneno makali na Rosell na hivi karibuni alidai kwamba hatahudhuria mechi yoyote ya Camp Nou kwa kipindi ambacho Rosell ataendelea kuwa madarakani. Lakini, Rosell anaamini hasira za Cruyff zimetokana na yeye kupuuza ushauri wa kocha huyo katika usajili aliotaka ufanyike na wao kumsajili Ronaldinho kutoka PSG mwaka 2003.
“Ilitokea kipindi kile ambacho nilikuwa Makamu Rais,” alisema Rosell.
“Alitoa ushauri wa kusajili wachezaji watatu; (Pablo) Aimar, (David) Albelda na (Roberto) Ayala, lakini sisi tuliwasajili Ronaldinho, Deco, Edmilson na (Rafael) Marquez. Hapo ndipo utata ulipoanza nadhani,” alisema.
“Kama hataki kuja Camp Nou, basi tutakuwa na nafasi moja ya wazi. Kama nitatakiwa kuitetea Barcelona, basi nitafanya hivyo.”
Msimu huu Barcelona ilimsajili Neymar kwa Euro 57 milioni, huku Cruyff akibeza kwamba staa huyo wa Brazil hataweza kucheza pamoja na Muargentina, Lionel Messi.
Comments
Post a Comment