Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Bw. Clement Mshana(kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo Pichani) kuhusu mkutano Mkuu wa mwaka wa Vyombo vya Utangazaji vya nchi Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC) unaotarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 21 october 2013 Jijini Arusha, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Kulia ni Mratibu wa Kanda wa Shirika hilo Bw. Joe Rugarabamu.
Picha na Hassan Silayo-MAELEZO
SHIRIKA LA UTANGAZAJI TANZANIA (TBC)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO MKUU WA MWAKA WA VYOMBO VYA UTANGAZAJI VYA NCHI ZA JUMUIA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA (SADC)
Chama cha Vyombo vya Utangazaji vya nchi zilizo Kusini mwa Afrika, kila mwaka hufanya Mkutano Mkuu (Annual General Meeting) katika nchi mojawapo mwanachama. Chama hiki kijulikanacho kama ‘SOUTHERN AFRICAN BROADCASTING ASSOCIATION’, kwa kifupi SABA, mwaka huu kimeipa heshima Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa mwaka.. Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ndiye mwenyeji wa mkutano huu wa 21 ambao utafanyika tarehe 21 hadi 24 Oktoba, 2013 katika ukumbi wa AICC, jijini Arusha
Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 21 Oktoba, 2013 na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Viongozi wengine watakaohudhuria ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Waziri wa Maliasili na Utalii, na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, pamoja na wajumbe kutoka nchi Mashirika wanachama wa SABA. Mkutano huo pia utahudhuriwa na mabalozi kutoka nchi za SADC, Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano katika nchi wanachama, vyombo vya utangazaji vya kimataifa, wawakilishi wa vyombo vya utangazaji vya nchini Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki na wataalamu wa masuala ya utangazaji na utalii.
Kauli mbiu ya mkutano huo Mkuu wa SABA ni ‘NAFASI YA VYOMBO VYA UTANGAZAJI KATIKA KUKUZA UTALII’. Washiriki wa Mkutano huo watajadili kwa kina mbinu na changamoto za kutumia vyombo vya utangazaji katika kukuza utalii. Tanzania itatumia fursa hii kuzidi kutangaza na kuhamasisha jamii kuhusu Maajabu Matatu kati ya Saba ya Asili ya Afrika yaliyoko Tanzania, ambayo ni Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro na Serengeti.
Wakati wa mkutano huo kutakuwa na mada mbalimbali za kitaalamu zitakazowasilishwa na kujadiliwa kuhusu teknolojia ya dijiti na fursa zake kwa vyombo vya utangazaji vya Afrika. Aidha masuala ya ubora wa maudhui ya vipindi, mikakati ya utangazaji wa kidijiti kwa televisheni na redio yatajadiliwa.
Nchi 14 wanachama wa SABA ni Afrika ya Kusini, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Kwa kuwa mkutano huu unafanyika nchini mwetu, nachukua nafasi hii kuwakaribisha wadau wote wa utangazaji na utalii kushiriki kwenye mkutano huu muhimu wa kimataifa. Kuhusu ushiriki tafadhali fuatilia matangazo ya mkutano huu yanayotolewa kwenye televisheni na redio za TBC.
Asanteni sana.
Clement Mshana
Mkurugenzi Mkuu, TBC
3 Oktoba, 2013.
Comments
Post a Comment