KIUNGO MATATA STEVEN MAZANDA: MAANDALIZI YA MAPEMA YAMETUPA MAFANIKIO, NAPENDA VIJANA WANAVYOCHEZA SOKA KWA SASA!!
Kiungo
jembe wa Mbeya City FC, Steven Mazanda (waliosimama, wapili kulia)
amesema hawana presha na kasi ya timu pinzani, mzunguko wa pili wako
fiti balaa!
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Kiungo
wa Mbeya City, Steven Mazanda, amesema siri ya mafanikio ya kikosi chao
katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu soka Tanzania bara uliomalizika
novemba 7 mwa huu na klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya tatu kwa
pointi 27 sawa na Azam fc katika nafasi ya pili ni maandalizi ya mapema
waliyofanya pamoja na nidhamu kubwa ya wachezaji kuanzia uwanjani na nje
ya uwanja.
“Unajua
sisi tulijiandaa mapema sana, na ndio maana unaona kikosi kinacheza
kitimu na kila mtu anavutiwa. Kiukweli kumekuwepo na changamoto za
ushindani, lakini tunaingia katka kila mechi kuhitaji ushindi”. Alisema
Mazanda.
Mazanda
ambaye amewahi kuzichezea timu za Tukuyu, Simba, Mtibwa na Kagera
Sugar, kabla ya kuisaidia Mbeya City kupanda daraja ameongeza kuwa
mzunguko wa pili hakika utakuwa mgumu kwao kwani timu nyingi zinajipanga
kujiweka sawa katika msimamo.
“Kuna
timu zitakuwa zinawania nafasi ya ubingwa, nyingine nafasi za katikati,
wakati hatari zaidi itakuwa mkiani ambao klabu zitakuwa zinawania
kukwepa mkasi wa kushuka daraja. Sisi tuko tayari kwa kupambana na hiyo
ndiyo kazi yetu”. Alisema Mazanda.
Kiungo
huyo mwenye uwezo mkubwa wa kukaba, kupanda na kushambulia pia, ni
mpigaji faulo mzuri amekiri kuwa vijana wamekuwa wakicheza soka safi
sana na kuonesha juhudi zao, lakini kwa yeye aliyecheza soka kwa muda
mrefu huwa hawampi presha akiwa dimbani.
“Nafurahi
sana kuona changamoto kubwa ya vijana wakiwa uwanjani, timu zote
zinazotumia damu changa zinafanya vizuri sana, kiukweli hawa makinda
wapewe nafasi ili sisi wakongwe tuwaoneshe jinsi mpira unavyochezwa”.
Alisema Mazanda.
Mazanda alisema kwa sasa kazi yao ni moja tu ambayo ni kujiandaa kwa mzunguko wa pili na lazima kieleweke.
“Tulivyoanza,
watu walisema nguvu ya soda, nadhani hata wewe mwenyewe ulisikia,
lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele, tulipata nguvu zaidi. Sasa
ahadi yetu ni kuonesha soka la uhakika”. Alisema Mazanda.
Ingawa umri umeenda lakini uzoefu unaonesha kuwa viungo huwa bora kwa jinsi umri unavyoenda.
Comments
Post a Comment