Dk. Zehlani ambaye huandika makala za afya, alichambua: “Ubovu wa mapafu ya Mandela ulisababishwa na Kifua Kikuu ambacho alikipata gerezani.”
Daktari huyo aliongeza: “Kuna mambo mengi husababisha maambukizi ya mapafu. Mgandamizo wa hewa kama njia ya upitishaji oksijeni na utoaji wa kaboni ni ndogo, kama kuna vimelea hatari vinavyoingia na kutoka kwenye mapafu au uingiaji wa wadudu wa Kifua Kikuu.
“Kwa kazi ngumu alizokuwa anafanya gerezani, lile vumbi, mtu anaumwa lakini hapati tiba muafaka, kwanza ni mshangao kuona amefikisha umri wa miaka 95, amejitahidi sana, kama mwili wake usingekuwa imara, angekufa kabla ya mwaka 1994.”
ZUMA ALIVYOLIHUTUBIA TAIFA
Usiku wa kuamkia jana, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, aliutangazia ulimwengu kupitia Televisheni ya Taifa ya Afrika Kusini kuhusu kifo cha Mandela akisema: “Mzee wetu amepumzika. Taifa letu limepoteza mtoto wake bora. Watu wa taifa letu wamempoteza baba yao. Ameondoka kwa amani.
Akaendelea: “Mawazo yetu yanarandana na mamilioni ya watu ambao walimkumbatia Mandela kama mtu wao na kuona kila kitu chake ni chao, hiki ni kipindi cha huzuni kubwa sana.
“Tuliona ndani yake kile ambacho tunahitaji na ndani yake tuliona mengi yenye manufaa kwetu. Nelson Mandela alituweka pamoja, kwa maana hiyo tutamkumbuka.”
AFIA NYUMBANI
Mandela alifariki dunia akiwa nyumbani kwake, Johannesburg, Afrika Kusini, baada ya mapafu yake kushindwa kufanya kazi.
Tofauti na mara nyingine ambazo Mandela alizidiwa na kukimbizwa hospitalini, awamu hiyo haikuchukua muda mrefu kwa nafsi kuacha mwili baada ya mapafu kufeli.
Kwa muda mrefu, Mandela alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya mfumo wa upumuaji, maradhi ambayo inaelezwa kwamba aliyapata kipindi akitumikia kifungo cha miaka 27 jela.
Mara kadhaa, Mandela alizushiwa kifo, kuna nyakati vyombo vya habari ulimwenguni vilijazana hospitalini alipokuwa amelazwa na kuripoti hatua kwa hatua kuhusu maendeleo ya afya yake, huku ikiaminiwa kwamba angekufa wakati wowote.
Siku zote anayejua siri ya kifo cha binadamu ni Mungu pekee, maana akiwa nyumbani akiendelea na matibabu madogomadogo, Mandela alifariki dunia na kuacha mshtuko na mshangao, maana imeonekana kama ‘ameondoka kimyakimya’ tofauti na matarajio ya awali.
MANDELA NI SHUJAA WA DUNIA
Rais wa Marekani, Barack Obama, anamuelezea Mandela kama kioo kwake na kwamba alijifunza siasa kupitia kiongozi huyo.
“Jinsi alivyoendesha harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, akakubali kufungwa jela kwa sababu ya kutetea haki na usawa wa wananchi wa Afrika Kusini, ilionesha kwamba siyo mbinafsi na alipambana kwa ajili ya wengi, hiyo ilinihamasisha kuipenda siasa,” Obama aliwahi kunukuliwa.
Mandela alipewa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1993 pia akatajwa kama mtu wa mfano kuwahi kutokea, maana ilidhaniwa kwamba baada ya kushinda kiti cha Urais wa Afrika Kusini mwaka 1994, angeweza kulipiza kisasi kwa Makaburu (Wazungu) waliowanyanyasa watu weusi nyakati za Utawala wa Ubaguzi wa Rangi nchini humo.
Kitendo cha kutolipiza kisasi, huku akiiongoza nchi hiyo kwa miaka mitano tu kwa haki na usawa kwa kila raia wa Afrika Kusini, ni mambo yaliyomfanya awe na thamani kubwa duniani.
Hata uamuzi wake wa kutotaka kung’ang’ania madaraka, umemfanya awe na heshima kubwa leo.
ALIPOTOKA
Alizaliwa Julai 18, 1918 katika kabila la machifu, kwenye Kijiji cha Mvezo, mjini Transkei katika Jimbo la Eastern Cape.
Alipewa jina la Rolihlahla ambalo kwa tafsiri ya Kabila la Xhosa maana yake ni msumbufu, akitajwa kuwa mantiki ya jina hilo ilijionesha namna alivyoisumbua Serikali ya Makaburu.
Akiwa na umri wa miaka nane, baba yake alifariki na kuanzia hapo alipelekwa kulelewa na Chifu wa Kabila la Thembu ambaye ndiye aliyeratibu ndoa yake ya kwanza.
Mwaka 1943, Mandela alitunukiwa Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini na ni nyakati hizo alijiunga na Chama cha African National Congress (ANC) ambacho alikiongoza kupigania usawa wa watu weusi wa Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye mwaka 1994 kuwa rais wa kwanza mweusi, akishinda kupitia tiketi ya chama hicho.
Mwaka 1948, Mandela alichaguliwa kuwa Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa ANC (ANC Youth League).
Mwaka 1962, baada ya kuendesha harakati nyingi za mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuhamasisha mgomo wa siku tatu, vilevile kusafiri nje ya nchi bila kuwa na kibali.
Mwaka 1963, nyaraka ya siri kuhusu Mandela inayoitwa Umkotho we Sizwe ilikamatwa, ikidaiwa kwamba ilikuwa na vipengele 70 vya kimapinduzi dhidi ya serikali.
MIAKA 27 JELA
Kutokana na makosa mbalimbali ambayo baadaye yalikuja kumfanya atajwe kama gaidi, yalisababisha afungwe jela miaka 27 kabla ya kuachiwa huru mwaka 1990.
Alitumikia miaka 18 kwenye Gereza la Robben Island kabla ya kuhamishiwa Pollsmoor nje ya Jiji la Capetown.
Mwaka 1988, alilazwa hospitalini baada ya kugundulika ana maambukizi ya Kifua Kikuu, ni ugonjwa huo ambao unatajwa kuchochea maradhi ya mapafu ambayo yamechukua uhai wake.
Februari 11, 1990, Mandela aliachiwa huru.
AANZA SIASA UPYA
Akiwa na umri wa miaka 71, Mandela alianza upya harakati za siasa baada ya kutoka jela ambazo zilimwezesha kushinda kiti cha urais mwaka 1994.
NDOA
Mandela alikumbana na migogoro ya ndoa, kwani alimtuhumu aliyekuwa mkewe, Winnie Mandela kwamba hakuwa mwaminifu, akamtaliki na kumuoa mjane wa aliyekuwa Rais wa Msumbuji, Samora Machel, Graca ambaye aliishi naye mpaka mwisho wa uhai wake.
Mke wake wa kwanza ni Evelyn Mase ambaye walizaa watoto wanne kabla ya kuachana, kisha akapata watoto wengine wawili na Winnie. Mandela, ameacha watoto watatu walio hai, kwani wengine watatu (wote mama ni yao ni Evelyn), walifariki dunia kabla ya baba yao.
Comments
Post a Comment