Iringa/Dar. Wakati mwili wa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ukitarajiwa kuzikwa leo, Serikali imesema kilichosababisha kifo chake ni ugonjwa wa figo.
Dk Mgimwa alifariki Januari Mosi, mwaka huu katika Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Pretoria nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile uliutaja ugonjwa huo mbele ya waombolezaji waliofika kuuaga mwili wake kwenye Viwanja vya Karimjee.
Likwelile alisema: “Marehemu Mgimwa alikwenda Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Afrika Kusini Novemba 3, mwaka 2013 kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake...baada ya uchunguzi, madaktari walimshauri alazwe kwa uangalizi zaidi na matibabu na kwamba aliendelea na matibabu ya figo hadi kifo chake.”
Aaagwa Dar
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya waombolezaji waliofika kwenye viwanja vya Karimjee kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Dk Mgimwa, pamoja na viongozi wengine wakiwemo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Spika wa Bunge, Anne Makinda, mawaziri, Mama Maria Nyerere na viongozi wengine wa vyama vya siasa.
Kikwete ambaye alikuwa wa mwisho kutoa heshima zake baada ya kuchelewa kufika kwenye viwanja hivyo akitokea Zanzibar, mara baada ya kufika alitia saini kitabu cha maombolezo na kutoa heshima za mwili kwa marehemu Mgimwa.
Kwa mujibu wa ratiba, leo Rais Kikwete pia anatarajiwa kuongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Iringa kwenye mazishi ya waziri huyo yanayotarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Magunga.
Salamu za Mbowe
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema Dk Mgimwa alikuwa mwelewa, mnyenyekevu na mstarabu.
“Kwa muda niliomfahamu Dk Mgimwa akiwa kwenye siasa, sikuwahi kumwona akikwaruzana wala kugombana, muda wote alikuwa mstaarabu na msikivu kwa kila mtu,” alisema.
Mbowe alisema viongozi wa kisiasa wanatakiwa kuiga mfano wake kwa kuacha chuki na malumbano yasiyokuwa na tija.
Comments
Post a Comment