MANCHESTER, ENGLAND
MREMBO Coleen Rooney anasubiri kwa hamu kubwa
mazungumzo ya mkataba mpya wa mumewe, Wayne Rooney wa kuendelea kubaki
klabu Manchester United. Taarifa zinabainisha kwamba mchezaji huyo
anaandaliwa mshahara wa pauni 300,000 kwa wiki.
Mrembo huyo anadaiwa kumtaka mumewe asaini mkataba
mwingine wa miaka mitano wa kubaki Manchester ili kuwasubiri watoto
wao; Kai, 4, na Klay mwenye umri wa miezi minane kuwa na umri mkubwa
kabla ya kuhama.
Mkataba ambao Manchester United inataka kumpa
Rooney una thamani ya pauni 65 milioni na utamfanya straika huyo kuwa
mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi England.
Kwa sasa analipwa kiwango sawa na mchezaji
mwenzake wa Manchester United, straika wa Kidachi, Robin van Persie,
pauni 250,000 kwa wiki.
Rafiki wa mrembo Coleen, 27, anasema: “Kitu
kikubwa Coleen hataki wahame kutoka Kaskazini Magharibi na jambo hilo ni
muhimu sana kwa Wayne. Hataki kuondoka eneo hilo na kutokana na kupokea
ofa nzuri ya pesa nyingi anaamini hilo ni jambo muhimu akabaki klabu
hapo.”
Manchester United imeipiga marufuku Chelsea kwamba
isithubutu kumfuatilia straika wao huyo kwa sababu hawawezi kumuuza kwa
wapinzani. Real Madrid pia inafukuzia saini ya staa huyo wa Old
Trafford.
Lakini, Coleen hayupo tayari kuona watoto wake
wakihamia London wangali wadogo hivyo, ukiweka kando Hispania.
Anachotaka yeye waendelee kubaki Manchester hadi hapo baadaye.
Familia hiyo inaishi Prestbury, Cheshire, na
wazazi wa Coleen, Colette na Tony wanaishi umbali wa maili 50 huko
Formby, Merseyside, karibu na familia ya akina Rooney.
Coleen amesema Rooney, ambaye alijiunga na
Manchester United akitokea Everton mwaka 2004, atapata shida sana
kutulia kama atacheza bila ya sapoti ya familia zao.
Lakini, kuna mtazamo tofauti wakati kocha David
Moyes akihaha na kuafiki mshahara wa pauni 300,000 kwa Rooney,
wachambuzi wa soka wanadhani Manchester United inapaswa kulichukulia kwa
hadhari suala la mchezaji huyo.
Staa huyo tayari anaonekana kuiringia Manchester
United kwa kuweka kando suala la kusaini mkataba mpya akisubiri hatima
ya klabu mwishoni mwa msimu kama itakuwa ndani ya nne bora na kama klabu
hiyo itafanya usajili wa mastaa wapya.
Comments
Post a Comment