Wizara
ya Maliasili na Utalii inapenda kuujulisha umma matokeo ya sensa ya
tembo iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu ili kuiwezesha
Serikali kutambua hali ya rasilimali ya wanyamapori ndani na nje ya
maeneo yaliyohifadhiwa.
Wizara
kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani na nje ya nchi imefanya sensa
katika Maeneo ya Mfumo ikolojia wa Selous – Mikumi na Ruaha – Rungwa
pekee kwa kuwa ni maeneo yenye tembo wengi nchini.
Matokeo
ya sensa hii yanaonyesha kwamba Mfumo wa ikolojia wa Selous-Mikumi kwa
sasa una tembo wapatao 13,084 na Ruaha–Rungwa una tembo wapatao 20,090.
Takwimu hizi zinaonesha kupungua kwa idadi ya tembo na hasa katika mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi ikilinganishwa na Sensa za awali.
Takwimu
za muda mrefu zinaonesha kwamba mwaka 1976 katika mfumo ikolojia wa
Selous–Mikumi kulikuwa na tembo 109,419. Idadi hii ilipungua kufikia
22,208 mwaka 1991 kutokana na wimbi la ujangili uliokuwepo katika
kipindi cha mwaka 1984 -1989. Hata hivyo, idadi hiyo iliongezeka na
kufikia 70,406 mwaka 2006 baada ya Operesheni Uhai iliyofanyika mwaka
1989 na 1990 na juhudi za kimataifa za uhifadhi ikiwemo kusitisha
biashara ya meno ya tembo.
Aidha,
idadi ya tembo nchini ilipungua hadi kufikia jumla ya tembo 38,975
mwaka 2009 na kuendelea kupungua hadi kufikia tembo 13,084 hivi sasa.
Hali
kama hiyo inaonekana pia katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha-Rungwa
ambapo sensa ya mwaka 1990 ilionesha kuwa na tembo 11,712 kutokana na
wimbi la
ujangili. Idadi hii iliongezeka na kufikia 35,461 mwaka 2006. Hata
hivyo, idadi hiyo imepungua na kubakia tembo 20,090 hivi sasa.
Kwa
matokeo haya inaonesha kuwa katika mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi
idadi ya tembo imepungua kwa asilimia 66 ikilinganishwa na idadi ya
mwaka 2009 ambapo kulikuwa na jumla ya tembo 38,975. na katika Mfumo
ikolojia wa Ruaha–Rungwa Tembo wamepungua kwa asilimia 36.5
ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009 ambapo kulikuwa na jumla ya tembo wapatao 31,625.
Kupungua
huku kunathibitishwa na idadi ya mizoga ya tembo iliyohesabiwa wakati
wa zoezi la sensa. Jumla ya mizoga 6,516 na 3,496 ilihesabiwa katika
mifumo ikolojia ya Selous-Mikumi na Ruaha–Rungwa. Katika zoezi hili
Wizara ilitumia vigezo vya uwiano wa mizoga na tembo hai waliohesabiwa
(carcass ratio) kubaini vyanzo vya vifo hivyo. Katika hali ya kawaida,
uwiano wa asilimia 7 – 8 unaashiria vifo vya asili kama vile ugonjwa na
uzee. Zaidi ya asilimia hiyo inaashiria vifo visivyo vya asili.
Sensa
iliyofanyika mwaka huu imeonesha uwiano wa asilimia 30 kwa mfumo
ikolojia wa Selous-Mikumi na asilimia 14.6 kwa Ruaha–Rungwa. Kwa mujibu
wa matokeo hayo, idadi kubwa ya vifo vya tembo vimetokana na vifo
visivyo vya asili.
Uchambuzi
wa kina umebainisha kuwa asilimia 95 na 85 ya mizoga iliyoonekana
katika mifumo ikolojia ya Selous-Mikumi na Ruaha–Rungwa ni ya zaidi ya
miezi 18 iliyopita.
Hii
inaonesha kuwa juhudi za makusudi zilizofanywa na serikali ikiwa ni
pamoja na kuimarisha doria na operesheni maalum mbalimbali za hivi
karibuni zimesaidia kupunguza wimbi la ujangili kwa kiasi kikubwa.
Aidha,
kukamatwa kwa meno ya tembo yenye uzito wa kilogramu 32,987 ndani na
nje ya nchi katika kipindi cha 2008 hadi Septemba 2013 ni ishara tosha
kuwa ujangili ni mojawapo ya sababu kubwa za kupungua kwa idadi ya tembo
nchini.
Sababu
nyingine ni kuongezeka kwa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa na
shoroba za wanyamapori. Mathalan, katika Pori Tengefu la Kilombero
ambalo ni sehemu ya ikolojia ya Selous – Mikumi, mwaka 2002 lilikuwa na
tembo 2,080, katika sensa ya mwaka huu, hukukuwa na tembo hata mmoja.
Ongezeko
la bei katika masoko ya biashara haramu ya meno ya tembo hususan katika
nchi za Mashariki ya mbali ni kichocheo na kisababishi kikubwa.
Kufuatia
hali hii, Wizara inaimarisha ulinzi wa wanyamapori kwa kushirikiana na
vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine za kanda na kimataifa
pamoja na kuelimisha na kushirikisha wananchi katika masuala mbalimbali
ya uhifadhi.
Ili
kuimarisha na kuboresha shughuli za uhifadhi, Wizara iko katika hatua
za mwisho za kuanzisha mamlaka mpya ya wanyamapori. Vilevile sheria za
uhifadhi zinapitiwa ili kuruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa kijeshi kwa
watumishi wa sekta ya wanyamapori.
Wizara
inapenda kuwatambua na kuwashukuru wafadhili wote waliofanikisha sensa
hii iliyogharimu kiasi cha dola za kimarekani 160,000ikiwa ni fedha za
serikali na wafadhili. Wafadhili hao ni Shirika la Misaada ya Kiufundi
la Ujerumani (GIZ) kupitia Frankfurt Zoological Society (FZS) na Shirika
la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kupitia Mradi wa TANAPA wa
SPANEST.
Imetolewa na
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Lazaro Nyalandu (MB)
10/01/2014
Comments
Post a Comment