Meneja
Mawasiliano wa TANAPA Pascal Shelutete akiongea na waandishi wa habari
jijini Arusha alipokutana nao kutoa ufafanuzi kuhusiana na kutokuwepo
kwa mpango wa kuikabidhi Hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa wawekezaji
kutoka Afrika Kusini kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila wiki
nchini hivi karibuni (Picha kwa hisani ya TANAPA)
Katika gazeti la Jamhuri Toleo Namba 129 Machi 25-31, 2014 kulikuwa na habari iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari “Nyalandu ‘auza’ Hifadhi” ambapo
maelezo ya habari hiyo yaliitaja Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuwa
inatarajiwa kukabidhiwa kwa wawekezaji kutoka nchini Afrika Kusini ikiwa
ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro
Nyalandu.
Shirika
la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi pamoja na
Hifadhi nyingine 15 nchi nzima linapenda kukanusha habari hiyo
iliyoandikwa kwa lengo la kupotosha umma kama ifuatavyo.
Mosi,
hakuna mpango wala uamuzi wowote uliopo au uliokwisha kufanywa wa
kuingia Mkataba wa Uendeshaji wa aina yoyote ile baina ya Shirika la
Hifadhi za Taifa na Mwekezaji yeyote kutoka nchini Afrika ya Kusini
ikiwa ni pamoja na African Parks Network waliotajwa katika habari
husika.
Pili,
Sheria inayosimamia uanzishwaji wa maeneo ya Hifadhi za Taifa ikiwemo
Katavi imelipa dhamana hii pekee shirika kusimamia maeneo haya kwa niaba
ya Watanzania na ni kinyume cha sheria kukabidhi kwa wawekezaji kwa
ajili ya usimamizi kama ilivyobainishwa katika habari hiyo.
Tatu,
Shirika la Hifadhi za Taifa bado linao uwezo thabiti wa kusimamia
uendeshaji wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi ili kuhakikisha rasilimali za
wanyama na mimea zinaendelea kutunzwa kwa miaka mingi ijayo kama ambavyo
imekuwa ikifanya tangu kuanzishwa kwa hifadhi hiyo mwaka 1974.
Aidha,
kama ambavyo shirika limekuwa likipanga katika mipango yake ya
maendeleo mwaka hadi mwaka, katika mwaka mpya wa fedha ujao shirika
limepanga kuongeza idadi ya watalii katika Hifadhi za Kusini ikiwemo
Katavi Saadani,
Mikumi na Ruaha. Mkakati huu utahusisha kuongeza ubora wa utoaji huduma
ikiwa ni pamoja na malazi ili kukuza utalii wa ndani.
Shirika
litafungua ofisi Jijini Dar es Salaam na kuimarisha ofisi za Mwanza na
Iringa ili watalii wapate taarifa za Hifadhi na kuweza kufanya
‘bookings’ kwa urahisi. Aidha, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa
masoko ya nje, Shirika sasa litaanzisha ‘Road shows’ mbalimbali kwa soko
la ndani na nchi za jirani. Vilevile, Shirika litaongeza kujitangaza
kupitia Mitandao ya Jamii, TV, majarida na tovuti ya Shirika itaboreshwa
katika kuarifu wadau masuala mbalimbali yanayojiri kwenye Hifadhi zetu.
Tayari
Shirika limeanzisha Kurugenzi mpya ya Utalii na Masoko kwa ajili ya
kutekeleza mkakati huu wa kuzifanya hifadhi za ukanda wa kusini kuvutia
watalii wengi zaidi.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
Comments
Post a Comment