JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika baadhi ya magazeti ya leo
tarehe 27 Juni, 2014 yameandika taarifa ambazo sio sahihi likiwemo
gazeti la Uhuru lenye kichwa cha habari “BILA KUPITIA JKT HAKUNA AJIRA
SERIKALINI na gazeti la Tanzania Daima lenye kichwa cha habari “IKULU:
RUSHWA YA NGONO IMEKITHIRI SERIKALINI”.
Magazeti yote haya yameandika
habari za kupotosha Umma kuhusu hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi aliyoitoa
tarehe 26/6/2014 katika mkutano wa Mwaka wa Wakurugenzi wa Utawala na
Rasilimali Watu, Makatibu Tawala uliofanyika mjini Dodoma. Magazeti hayo
yamejenga taswira kwamba Katibu Mkuu Kiongozi alitoa taarifa kwamba
“Hakuna ajira bila kupitia Jeshi la Kujenga Taifa” na “Rushwa ya ngono
imekithiri Serikalini”.
Serikali inapenda kutoa ufafanuzi
kwamba taarifa hizo siyo za kweli wala hazielezi taarifa halisi
aliyoigusia Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Ombeni Sefue. Katika
hotuba yake alisema “Aidha, ningependa mjue kuwa kuanzia sasa tutaweka
mkazo mkubwa sana kwenye sifa ya uzalendo kwenye ajira Serikalini.
Hatuwezi kuwa na Watumishi wa Umma ambao hawana uzalendo.Pale ambapo
waombaji kazi kwenye Utumishi wa Umma wana sifa zote sawa, lakini
wakawepo wale ambao wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa watapewa
kipaumbele.lakini narudia, kipaumbele hicho kitumike pale tu ambapo sifa
zingine zote ziko sawa, na si vinginevyo”.
Kuhusu suala la rushwa ya ngono
lililoripotiwa na gazeti la Tanzania Daima, si kweli kwamba Katibu Mkuu
Kiongozi alisema kumekuwa na ongezeko au kukithiri kwa rushwa ya ngono
katika utoaji wa ajira serikalini. Alichokisema Katibu mkuu kiongozi ni
kwamba “Lakini bado malalamiko yanasikika kuwa ati huwezi kuajiriwa
kwenye Utumishi wa Umma isipokuwa kama unajulikana au unatoa rushwa, ama
ya fedha au ya ngono. Jambo hilo linanisononesha sana. Mimi naamini
mambo hayo yamepungua sana. Lakini kama yanafanyika, ni kinyume kabisa
na Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma na lazima tulio
katika ukumbi huu tuyapige vita kwa bidii zote, bila kuoneana haya, hadi
wananchi waone kuwa kweli hayapo. Tusipuuze hata kidogo malalamiko ya
wananchi, bali tujichunguze na tuchunguzane, ili kama mambo hayo bado
yapo, kwa pamoja tuazimie kuyakomesha kabisa kwenye Utumishi wa Umma”.
Hotuba halisi ya Katibu Mkuu Kiongozi inaweza kupatikana
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI – MAELEZO
27/6/2014
Comments
Post a Comment