Mahmoud Ahmad,Arusha.
WATOTO waishio kwenye mazingira
magumu na yatima hususani wanaoishi na virusi vya ukimwi wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kunyanyapaliwa na wazazi na hata
walimu mashuleni hali ambayo imekuwa ikiwawia vigumu watoto hao
kuendelea na masomo.Aidha unyanyapaa kwa watoto yatima wanaoishi na
virusi vya ukimwi imekuwa ni changamoto kubwa kwao ambapo asilimia kubwa
ya watoto wamekuwa wakikosa haki zao za msingi hususani elimu kutokana
na hali hiyo.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi
wa shirika la Sorode Organization la jijini hapa, Sophia Justine wakati
akizungumza na watoto na walezi waliohudhuria katika harambee ya
kuchangia bweni kwa ajili ya watoto yatima wa kike wanaolelewa katika
kituo cha Faraja ambapo shs 1 milioni zilipatikana huku zikihitajika shs
50 milioni.
Alisema kuwa, kumekuwepo na
unyanyapaa wa hali ya juu unaofanywa na walimu katika shule mbalimbali
baada ya kupewa taarifa kuhusu watoto hao hali ambayo imekuwa
ikisababisha watoto hao kutengwa na wengine na hata wakati mwingine
kuchukiwa kabisa na walimu na wazazi kwa ujumla.
Sophia alisema kuwa, watoto hao
wanahitaji kupatiwa haki zote za msingi kama wanavyopata watoto wengine
badala ya kunyanyapaliwa na kutengwa na jamii kama watoto wasiofaa na
kustahili kama wengine kitendo ambacho kimekuwa kikiwapa wakati mgumu
kuishi katika jamii.
‘sisi shirika letu hili tumekuwa
tukitoa elimu kwa jamii mbalimbali ikiwemo vituo mbalimbali vya watoto
yatima ili kuweza kujua haki za mtoto ,na changamoto zinazowakabili ndio
maana leo tukaamua kuandaa harambee hii ambayo ndo mwanzo tu lengo ni
kuhakikisha fedha za bweni zimepatikana kwa ajili ya kusaidia watoto
hawa wa kike’alisema Sophia.
Naye Mkurugenzi wa kituo hicho cha
kulelea watoto yatima cha Faraja ,Faraja Maliaki alisema kuwa, kituo
hicho kina jumla ya watoto 200 ambapo kati ya hao watoto 30 wanaishi na
virusi vya ukimwi na watoto 48 wakiwa hawajulikani kabisa walipotokea
wala makabila yao kutokana na kuokotwa baada ya kutupwa baada ya
kuzaliwa.
Alisema kuwa, kituo hicho kimekuwa
kikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa bweni la
wasichana ambapo kituo kina idadi ya wasichana 103 ambao wamekuwa na
uhitaji huo wa bweni.
Faraja aliongeza kuwa, watoto hao
wamekuwa wakilala chini na wengine kusongamana kwenye kitanda kimoja
kutokana na kutokuwa na bweni ,hivyo aliomba wadau mbalimbali kujitokeza
kuchangia bweni la watoto hao ambao wanaendelea kukua siku hadi siku.
Aidha alielezea changamoto
nyingine kuwa ni pamoja na malazi, chakula,mavazi,kwani wakati mwingine
wamekuwa wakila mlo mmoja tu kwa siku huku idadi yao ikiendelea
kuongezeka kila siku
Comments
Post a Comment