*Askofu Niwemugizi ataka UKAWA warudi bungeni mwezi ujao, asema siyo ombi
……………………………………………………………
WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini kote nchini na wananchi
waungane pamoja ili kuombea uchaguzi mkuu wa viongozi wakuu wa Rais,
wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Ametoa wito huo leo mchana
(Jumanne, Julai mosi, 2014) wakati akizungumza na maelfu ya waumini na
viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya Jubilei ya miaka 25 ya Askofu
Mkuu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarsicius Ngalalekumtwa
katika uwanja wa Kichangani wa Kanisa Kuu la Kihesa.
“Maaskofu wote mliopo hapa, najua
mnavyoipenda Tanzania… kila kanisa lina sala maalum ya kuliombea Taifa
na viongozi wake, ninawaomba viongozi wetu mliombee Taifa letu ili mambo
yaende salama na hasa uchaguzi wa mwakani,” alisema.
Akirejea mahubiri yaliyotolewa
kwenye ibada hiyo na Mhashamu Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo Katoliki
la Tabora ambaye alitoa mfano wa Daudi na Goliathi, Waziri Mkuu
alimfananisha Goliathi na masuala ya rushwa, ubinafsi na tabia ya
viongozi kutojali wananchi wa hali ya chini.
“Viongozi tusipokuwa waadilifu,
tukawa wala rushwa na hatujali wananchi wa hali ya chini tutakuwa sawa
na Goliathi. Nawasihi sana ombeeni Taifa hili na uchaguzi mkuu ujao ili
Mungu atupe Daudi atakayeweza kuliongoza Taifa hili na kulipeleka
kunakostahili,” alisema huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu ambaye alihudhuria
sherehe hizo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, ametumia fursa hiyo pia
kuwaomba wote kwa pamoja waendelee kuliombea Taifa katika kipindi hiki
cha mchakato wa kuandaa Katiba Mpya. “Watanzania wote tuwe na moyo wa
kuvumiliana na kupendana. Tumuombe Mungu atuwezeshe kupata Katiba mpya
katika hali ya maelewano na amani. Tuombee Taifa na tuombee Watanzania
ili tusije tukatoka katika mstari.”
Alisema ushauri uliotolewa na
Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severini Niwemugizi wa kuwataaka wajumbe
wa Bunge Maalum la Katiba warejee mara moja ni wa muhimu. “Ushauri wa
Baba Askofu ni wa makini, turudi tukabishane pale ndani, lakini pamoja
na yote sheria inasema mwamuzi wa mwisho ni Watanzania kupitia kura ya
maoni. Wale tuliopewa dhamana ya kupitia rasimu turudi pale tuikamilishe
ili Watanzania waweze kupata fursa ya kupiga kura ya maoni,” alisema.
Mapema, akiwasilisha salamu kutoka
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini Niwemugizi
wa Jimbo la Ngara aliwataka wajumbe wa Bunge maalum la Katiba kurejea
kwenye mkutano wake uliopangwa kuanza Agosti 5, mwaka huu.
“Ninatumia neno kuwataka na siyo
kuwaomba warejee bungeni mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au kufanya
mizengwe mingine na kutupatia Katiba isiyotufaa, nitawaomba Watanzania
wote tuweke uzalendo mbele na kuikataa rasimu ya Katiba itakayoletwa na
pia tuwanyime uongozi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Aliwataka Watanzania wajitokeze
kwa wingi wakati wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.
“Watanzania tuna tabia ya kudharau siasa. Tusidharau masuala ya siasa
kwa sababu ni muhimu na yanagusa maisha yako na yangu, yanagusa maisha
ya watoto wako,” alisema.
Sherehe hizo za jubilei ya miaka
25, zilihudhuriwa na maaskofu 19 kutoka majimbo mbalimbali ya kanisa
katoliki hapa nchini, wawakilishi wa maaskofu watatu na abate mmoja.
Viongozi wa kitaifa waliohudhuria ni Spika wa Bunge, Mama Anne Makinda;
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa; Waziri Mkuu mstaafu,
Edward Lowassa na baadhi ya wabunge wa mkoa wa Iringa.Askofu Ngalalekumtwa (66) alipata upadrisho Aprili 7, 1973 huko San Ginesio, Camerino, nchini Italia na kupata daraja ya uaskofu mwaka 1988 ambapo alisimikwa rasmi Januari 1989 kuwa Askofu wa Jimbo la Sumbawanga
Comments
Post a Comment