Maafisa wa polisi nchini Kenya wanasema
wamemnasa mshukiwa mkuu wa Al-Shabaab mjini
Nairobi. Mshukiwa huyo alikuwa nchini Kenya
kutafuta matibabu.
Duru zingine zinasema kuwa alikuwa mwanahabari
zamani na anashukuwa kujihuhusisha na mauaji ya
waandishi wa habari wa Somali huko Mogadishu.
Ni nadra kunasa washukiwa kama hawa
wanaoingia nchi jirani ya Kenya kupitia mipaka yake
ambayo bado haina ulinzi wa kutosha.
Mshukiwa huyo anadhaniwa kuwa Hassan Hanafi
na amekuwa akizuru Kenya mara kwa mara.
Maafisa wa polisi wameambia BBC kuwa alitiwa
nguvuni siku chache zilizopita na anahojiwa na
maafisa wa kitengo maalum cha polisi
kinachoshughulikia maswala ya ugaidi.
Maafisa wa Usalama wa Somali wamesema kuwa
ushirikiano kati ya majasusi wa Kenya na Somali
ndiko kulipelekea au kuwezesha kukamatwa kwa
mshukiwa huyo ambaye anadai ameshikwa
kimakosa na kufananishwa na mtu mwingine.
Hanafi anashukiwa kutekeleza au kufadhili mauaji
ya wanahabari mjini Mogadishu. Zaidi ya
wanahabari 20 wameuwawa katika kipindi cha
miaka mitatu iliyopita nchini Somalia.
Inaaminika kuwa Hanafi alijiunga na Al-Shabaab
mwaka 2006, baada ya Ethiopia kuondoa mamlakani
muungano wa mahakama za kiislamu.
Baadaye Hanafi alifanya kazi katika kituo cha Redio
cha Andalus, ambacho hutumiwa kama ni kipaza
sauti cha al-Shabaab nchini Somalia, na hatimaye
kujiunga na mrengo wa Al-Shabaab unaotumia
silaha hatari.
Comments
Post a Comment