


Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Tanzania imepata fursa ya
kuwakutanisha wanasayansi kutoka nchi mbalimbali za Afrika na duniani
katika kongamano la 25 la Wajiolojia litakalokwenda sambamba na mkutano
wa tatu wa kimataifa wa mtandao wa wanasayansi vijana.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Jiolojia Tanzania (GST), ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya
maandalizi ya makongamano hayo, Profesa Abdulkarim Mruma, ameeleza kuwa,
kongamano la Wajiolojia litafanyika tarehe 15-16 Agosti, 2014,
likijikita katika
kujadili masuala ya Jiolojia na
namna Afrika inavyoweza kunufaika na taaluma hiyo kupitia sekta za
nishati, madini, maji, utalii, na masuala mengine yanayohusu sekta hiyo.
Aliongeza kuwa, kutokana na mada
mbalimbali zitazowasilishwa, na tafiti mbalimbali zitakazoainishwa
katika kongamano hilo la wajiolojia, zitasaidia kuziwezesha nchi za
Afrika kutangaza na kuhamasisha maeneo ya uwekezaji kupitia sekta za
madini, mafuta, gesi ikiwemo kuendeleza masuala ya utalii na kuangalia
namna inavyoweza kurithisha taaluma hiyo kwa kizazi kijacho.
“Tanzania ina masuala mengi ya
kijiojia, utafiti mwingi wa kisayansi kupitia taaluma hii, umefanyika
Tanzania, hivyo lazima tuiambie dunia kuhusu masuala ya kijiolojia na
utalii lakini hasa kile tulichonacho hapa kwetu kwa maendeleo yetu na
dunia,” aliongeza Mruma.
Aliongeza kuwa, zipo tafiti ambazo
zimefanywa na kampuni mbalimbali zinazofanya utafiti wa mafuta vikiwemo
vyuo vikuu mbalimbali kutoka Afrika ambazo zinatarajiwa kuwasilishwa
katika kongamano hilo.
Akielezea kuhusu kongamano la
vijana wanasayansi litakalofanyika kuanzia tarehe 11-14 mwezi huu,
Profesa Mruma alieleza kuwa, linafanyika kwa mara ya 3 tangu kuanzishwa
kwake mnamo mwaka 2009 na kwamba, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba
masuala ya sayansi ya dunia yanarithishwa ipasavyo katika kizazi kijacho
kwa lengo la kuendeleza rasilimali asilia zikiwemo mafuta, nishati ya
jotoardhi ikiwemo kuendeleza sayansi ya jiolojia kwa vijana kwa
maendeleo ya Afrika na dunia.
Aliongeza kuwa, kongamano hilo
litawashirikisha vijana wanasayansi kutoka katika nchi 45 Afrika na
mabara mengine na litatoa fursa kwa vijana wanasayansi kujadili masuala
mbalimbali ya kisayansi.
Naye Rais wa vijana wanasayansi
duniani, Meng Wang, alieleza kuwa, kongamano la vijana ni muhimu kwa
Afrika na hususani Tanzania kutokana na kuwa ni miongoni mwa nchi
zenye utajiri mwingi wa masuala ya kijiolojia na masuala ya utalii.
“Mengi yanayotarajiwa kuzungumzwa
katika makongamano haya yanaigusa Tanzania moja kwa moja, hii ni fursa
kubwa hasa kwa vijana wanasayansi na wasio wanasayansi kutokana na
kwamba jambo hili litachangia kujenga ari ya vijana kuingia katika
taaluma hii”, alisisitiza Wang.
Akieleza zaidi kuhusu kongamano la
vijana Mwenyekiti wa mtandaohuo wa vijana kwa upande wa Tanzania
Steven Nyagonda, alieleza vijana, waliona ipo haja ya kukutana kuangalia
namna masuala mbalimbali yanayoikabili dunia kupitia taaluma ya sayansi
ili kuunganisha jitihada za kizazi kilichopo na kijacho jambo ambalo
litawezesha kizazi kijacho kuirithi taaluma hiyo.
Aliongeza kuwa, kongamano hilo
litaangalia masuala mbalimbali ikiwemo kujadili matatizo yanayotokana na
taaluma hiyo, kupata uzoefu wa namna nchi nyingine duniani zinavyotumia
sekta ya nishati, namna elimu ya sayansi inavyoweza kuisaidia dunia,
katika mazingira, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na masuala mengine
yanayohusu dunia kupitia sayansi na jiolojia.
“Zaidi pia tunalenga kuwavutia
vijana wengi wapende masomo ya sayansi hususani somo la hisabati, lakini
zaidi sisi vijana wanasayansi wa Tanzania tunataka vijana wa kitanzania
waipende sayansi,” alisisitiza Nyagonda.
Aliongeza kuwa, zaidi ya tafiti
400 kutoka kwa vijana wanasayansi sehemu mbalimbali duniani
zimewasilishwa kwa kamati ya vijana ya dunia, ambapo kati yake tafiti 50
ziliwasilishwa na vijana wanasayansi wa watanzania.
Makongamano yote la Wajiolojia
Afrika na wanasayansi vijana kutoka nchi mbalimbali duniani yanatarajiwa
kufunguliwa rasmi tarehe 11 Agosti, 2014, na Makamu wa Rais wa
Jamhuri Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohamed Gharib Bilal akimwakilisha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Comments
Post a Comment