JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema limewakamata watu 71, silaha nne na dawa za kulevya katika oparesheni ya.......... mwishoni mwa mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema Desemba 24 mwaka huu, maeneo ya Ubungo Kibo, Kinondoni, Polisi walipata taarifa kutoka kwa mwananchi ambapo walifanikiwa kumkamata mfanyabiashara, Peter Massawe (25).
Kova alisema Massawe ni mfanyabiashara wa duka la nguo na mkazi wa Ubungo Rombo alikutwa na bastola aina ya Taurus, yenye namba 801340 iliyotengenezwa nchini Brazil ikiwa na risasi mbili na maganda ya risasi matatu.
Kwa mujibu wa Kova, mtuhumiwa alipohojiwa alidai kuwa silaha hiyo ililetwa na Ismail Mcharo (29), dereva wa bodaboda, mkazi wa Kimara Kilungule kwa ajili ya hifadhi baada ya kuitumia katika tukio la uporaji lililotokea maeneo ya Selander Bridge.
Pia alisema watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Matola Rashid (30) muuza mkaa na mkazi wa Kimara Baruti na Fitina Ramadhan (43) mkazi wa Magomeni.
‘’Mahojiano hayo pia yalisaidia kupatikana kwa silaha nyingine ambazo ni shotgun mbili, bastola moja, pikipiki tatu na simu mbili za mkononi,’’alisema Kova.
Alisema watuhumiwa wanahojiwa na kwamba upelelezi wa shauri hilo utakapokamilika jalada la kesi litapelekwa kwa mwanasheria wa serikali ili sheria ichukue mkondo wake.
Alifafanua kuwa jeshi hilo linaendelea kukabiliana na athari za dawa za kulevya ambapo jumla ya watuhumiwa 68 ambao ni wasambazaji wa dawa hizo, walikamatwa.
Aidha, wamekamata magunia manne ya bangi, kete 236 na misokoto 174, mtambo wa kutengenezea gongo pamoja na lita 50 za pombe haramu ya gongo.
Comments
Post a Comment