Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa ataanza ziara ya kuzunguka nchi nzima kuwashukuru Watanzania kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 na kesho atakuwa Tanga.
Katika ziara hiyo, Lowassa ataambatana na viongozi waandamizi wa Chadema na Ukawa kuwashukuru wananchi kwa namna walivyounga mkono upinzani na ajenda nzima ya mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imesema kiongozi huyo atatoa shukrani zake kwa wananchi kwa jinsi wanavyoendelea kuweka matumaini yao kwa upinzani.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba wananchi bado wanaamini kwamba upinzani ndiyo nguzo imara wanayoitegemea katika kuwaletea mabadiliko ya kweli kwa ajili ya maendeleo yao na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
“Wananchi wanastahili shukrani kwa imani hiyo kubwa ambayo ni ishara ya wazi kuwa matumaini yao kwa miaka mingine mitano yatasimamiwa na kuongozwa na upinzani imara kupitia Ukawa,” alisema Makene katika taarifa hiyo.
Alisema mbali na kupiga kura nyingi katika nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita, wananchi waliwachagua wabunge wengi wa upinzani wanaotokana na Ukawa. Alisema wabunge hao wameongeza nguvu kubwa ndani ya Bunge hususan kupitia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo itakuwa serikali mbadala.
Pia, alisema wananchi wameviamini vyama vya upinzani ili kusimamia na kuongoza halmashauri 34 nchi nzima, ikiwa moja ya misingi imara katika kupigania mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka.
Comments
Post a Comment