Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amezungumzia kasi aliyoanza nayo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli pamoja na baraza lake la mawaziri.
Akizungumza jana na mwandishi wa habari wa Azam TV, Mbowe alisema kuwa rais Magufuli ameanza vizuri kiutendaji na kwamba ameanza kuzifanyia kazi hoja zilizokuwa zikihubiriwa na Chadema ndani na nje ya Bunge.
“Hoja ya kubana matumizi ya serikali, hoja ya kupunguza sherehe za kitaifa, hoja ya kupunguza safari za nchi za nje kwa viongozi wetu, hoja ya kupunguza watumishi wa umma ambao hawana umuhimu, hoja ya kuwa na serikali ndogo. Haya mambo tulizungumza siku zote na hawa hawa wa Chama cha Mapinduzi ndio waliokuwa wanayapinga haya,”alisema Mbowe.
Mbowe alieleza kuwa dhana ya upinzani sio kupinga kila kitu kinachofanywa na serikali hivyo chama chake hakitakuwa tayari kupinga mambo mema yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano kama baadhi ya watu wanavyotarajia, bali kitajikita katika kujadili na kuibua hoja za msingi.
“Kuwa mpinzani sio kupinga kila jambo linalofanyika hata kama likiwa jema. Sasa sisi kama kambi rasmi ya upinzani bungeni na hata nje ya bunge ni wajibu wetu katika wakati wote ule kuhakikisha tunaisimamia serikali ili anachokisema rais kweli kitekelezwe kwa vitendo na isiwe hoja ya rais pekee,”alisema.
Hata hivyo, Mbowe alikosoa uteuzi wa baadhi ya mawaziri katika baraza la serikali ya awamu ya tano hususan Dk. Harison Mwakyembe ambaye wizara ya Uchukuzi aliyokua akiiongoza awali imekumbwa na sakata la upotevu wa makontena bandarini na Profesa Sospeter Muhongo ambaye amerudishwa katika wizara ya Nishati na Madini baada ya kujiuzulu katika nafasi hiyo wakati wa serikali ya awamu ya nne kufuatia sakata la Escrow.
Msikilize Mbowe akiongea hapo chin
Msikilize Mbowe akiongea hapo chin
Comments
Post a Comment