Waziri Wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu Atembelea MSD...... Aahidi Kuwa Balozi Wao Na Kuwatatulia Changamoto Zinazowakabili Ikiwepo Deni Wanaloidai Serikali
Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu jana alitembelea Makao Makuu ya Bohari ya Dawa (MSD) na kuahidi kuwa balozi wa kuhakikisha deni la serikali linalipwa ili......... kuiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Waziri huyo alieleza hayo baada ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu kueleza kuwa ukosefu wa fedha na deni la serikali ni changamoto kubwa inayoathiri utekelezaji mzuri wa majukumu ya MSD.
Mbali na hilo, Waziri wa Afya alisema mbali na deni hilo, hata kiasi cha fedha kinachotengwa na serikali kwaajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati na kununua dawa hakitoshelezi mahitaji, hivyo lazima suala hilo lifanyiwe kazi mapema, huku akisisitiza hata kiasi hicho kidogo kinachopatikana kitumike vizuri.
Katika hatua nyingine aliishauri Bohari ya Dawa kuanza utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, kuhakikisha dawa muhimu zinapatikana wakati wote na kuiagiza MSD itangaze kwenye vyombo vya habari dawa zote ambazo zinapelekwa vituoni, zahanati na kwenye hospitali, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alieleza kuwa tayari MSD imeshaanza kubandika kwenye mbao za matangazo za hospitali orodha ya dawa inazofikisha.
Waziri huyo ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Donald Mbando na watendaji wengine pia alitembelea maghala ya kuhifadhia dawa ya MSD, jengo la ofisi linalojengwa pamoja na kuwa na mkutano na menejimenti ya MSD, ambapo pamoja na mambo mengine aliipongeza MSD kwa hatua iliyofikia ya kuweka nembo ya GOT kwenye vidonge vyake ili kudhibiti upotevu wa dawa za serikali pamoja na kuanzisha maduka ya dawa Muhimbili, na mengine yanayotarajia kufunguliwa hivi karibuni mkoani Mbeya, Arusha na Mwanza.
Waziri Ummy Mwalimu alihitimisha kwa kusema kuwa ajenda yake kuu ni upatikanaji wa dawa kwa wakati, kama rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alivyoaainisha, hivyo MSD itekeleze majukumu yake ipasavyo kwani mafanikio ya MSD ni mafanikio kwake pia.
Comments
Post a Comment