WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ameuagiza uongozi wa mkoa wa Kagera,Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) na ...............vyombo vya dola, kuwashughulikia wala rushwa katika mradi ya umeme vijijini.
Amezitaka taasisi hizo na uongozi huo, kuchunguza na kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo katika mradi huo, unaosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ili wawachukulie hatua ikiwamo kuwafikisha mahakamani.
Alitoa kauli hiyo jana baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi na madiwani wanne wa Halmashauri ya wilaya ya Karagwe , wakiongozwa na Mbunge wao, Innocent Bashungwa, ambapo walisema wafanyakazi wa kampuni hiyo wamekuwa wakitoa umeme kwa watu wanaowapatia fedha za pembeni na kusababisha hata ramani ya ufungaji umeme kutofuatwa.
Walisema kwa nyakati tofauti kuwa watu wanaojitambulisha kuwa wanafunga umeme vijijni, wamekuwa wakiwataka wananchi watoe chochote kuanzia Sh 75,000 na kuendelea wakati wameishalipia Sh 27,000 zinazotakiwa kupata huduma hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella alisema amejaribu kufanya utafiti na kugundua kuwa hali hiyo imekuwa ikisababishwa na usimamizi hafifu wa kampuni inayosimamia mradi wa REA.
Wakati huohuo Waziri Muhongo ametaka uongozi wa Shirika la Umeme (Tanesco) mkoa na wilaya ya Karagwe na mkandarasi anayehusika na mradi wa REA, kujibu tuhuma hizo kama wameshazisikia na wamezitatua vipi.
Mhandisi Mshauri wa kampuni ya Urbanand Rural inayoshughulikia ufungaji umeme wa REA eneo hilo, Julius Kateti , alithibitisha kuwepo kwa udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyakazi wake wasio waaminifu.
Alisema kutokana na hilo, mpaka sasa ameshawafukuza kazi zaidi ya wafanyakazi 100 kati ya 680 huku kesi nane zikiwa Polisi.
Baada ya jibu hilo, Muhongo alisema kuwa tatizo hilo limeonekana ni la mkoa mzima na ndipo aliagiza Mkurugenzi wa Usambazaji wa Umeme nchini kutoka REA makao makuu, kufika mkoani Kagera mara moja ili kukaa na uongozi wa Tanesco na wa mkoa wa Kagera kuhakikisha wanatatua masuala hayo.
Baada ya jibu hilo, Muhongo alisema kuwa tatizo hilo limeonekana ni la mkoa mzima na ndipo aliagiza Mkurugenzi wa Usambazaji wa Umeme nchini kutoka REA makao makuu, kufika mkoani Kagera mara moja ili kukaa na uongozi wa Tanesco na wa mkoa wa Kagera kuhakikisha wanatatua masuala hayo.
Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Amos Maganga alimweleza mkandarasi wa REA kuwa ikibainika alichepusha mradi na kupeleka nje ya kilometa 453 za awamu hii kinyume cha mkataba, Tanesco haitatoa fedha ya Serikali kulipia ukiukwaji huo, bali mkandarasi atawajibika mwenyewe.
Akifafanua hilo, Profesa Muhongo alisema serikali imeweka azimio kuwa kampuni itakayobainika kunyanyasa wananchi, haipaswi kupata kazi tena katika awamu zijazo, kwani Watanzania wamechoka na ahadi zisizotekelezeka.
Comments
Post a Comment