Balozi Seif Ali Iddi atoa Taarifa Rasmi ya Maadhimisho ya Sherehe za Mikaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yatafanyika kama kawaida na kupangwa kuanza rasmi leo jumapili ya Tarehe 3 Januri 2016.
Alisema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba katika muda wote wa maandamisho hayo kunakuwa na hali ya utulivu na usalama mkubwa katika maeneo yote ya Visiwa vya vya Unguja na Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alisema hayo wakati akitoa Taarifa rasmi ya ratiba ya maadhimisho ya sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar mbele ya Wana Habari hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema suala la upande wa Upinzani kuzisusia sherehe za Mapinduzi kwa kisingizio cha Rais aliyepo madarakani si halali ni muendelezo wa kuwapotosha Wananchi walio wengi nchini.
Balozi Seif alifafanua kuwa Rais wa sasa Dr. Ali Mohammed Shein ataendelea kuwa rais hadi yule atakayechaguliwa rasmi na kihalali na Wananchi ale kiapo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kama ilivyokwishatolewa ufafanuzi na wanasheria walio wengi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Miradi yote ya Maendeleo ipatayo 24 ambapo 16 ikiwa imekamilika na Minane inatarajiwa kuwekwa mawe ya msingi imehusishwa katika maadhimisho hayo itakayoanza Jumatatu ijayo.
Alisema madhimisho hayo yataanza rasmi leo Jumapili ikiwa ni siku maalum kwa kazi za usafishaji wa masingira katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ukilenga zaidi katika sehemu za kutolea huduma za kijamii kama Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na masoko.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alifahamisha kwamba ingawa zoezi hilo hufanyika kila zinapoanza sherehe za Mapinduzi lakini mwaka huu juhudi malum zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha maeneo yote yanakuwa katika hali ya usafi muda wote.
Akigusia suala la hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ambalo limekuwa agenda kubwa kwa baadhi ya watu wakiwemo hata wanasiasa nchini wakiendelea kupotosha Wananchi Balozi Seif alisema Taarifa rasmi ya vikao vinavyowakutanisha Viongozi wa juu kulijadili suala hilo itatolewa rasmi mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
Hata hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio yenye mamlaka ya kuendesha na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema kwa vile tume hiyo kupitia Mwenyekiti wake haikuridhika na mazingira yaliyojichomoza wakati wa zoezi la kupiga kura na kulazimika kufuta Uchaguzi pamoja na matokeo yake yote Taasisi hiyo hiyo ndio yenye uwezo wa kuitisha uchaguzi mwengine kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.
Akijibu baadhi ya maswali ya Waandishi wa Habari Balozi Seif alisema katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 iko wazi na kutoa mamlaka kwa tume ya uchaguzi ya Zanzibar kupanga uchaguzi mwengine kufuatia kufutwa kwa ule wa mwezi oktoba mwaka 2015.
Comments
Post a Comment