Ikulu Yamjibu Dk Makongoro Mahanga Aliyemtuhumu Rais Magufuli Kuunda Serikali Kubwa Tofauti Na Alivyoahidi
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema ameshangazwa na kauli ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongo Mahanga kuwa wingi wa makatibu wakuu unakinzana na dhana ya kupunguza ukubwa wa Serikali alioahidi Rais John Magufuli.
Juzi mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Segerea (CCM) alisema kuteua makatibu wakuu 27 ni sawa na kuwa na wizara 27 badala ya 15 kama inavyoelezwa.
Dk Mahanga alisema huko si kupunguza ukubwa wa Serikali bali ni kuongeza ukubwa wake na kwamba wizara ni ofisi ya katibu mkuu na si ofisi ya waziri.
Lakini, Balozi Sefue alipotafutwa kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya Dk Mahanga, alisema kauli ya kiongozi huyo imemshangaza.
“Kwa mtu aliyekuwa naibu waziri kwa muda mrefu sana, inashangaza hajui kuwa makatibu wakuu si sehemu ya Baraza la Mawaziri,” alisema Sefue.
“Idadi yao si kipimo cha ukubwa au udogo wa Baraza la Mawaziri,”alisema Balozi Sefue.
Sefue aliongeza kuwa idadi ya makatibu wakuu na naibu wao waliokuwapo kwenye Serikali iliyopita na waliopo sasa ni tofauti, kwa kuwa wamepungua.
“Jumla ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa Serikali iliyopita ilikuwa 54. Hivi sasa wako 49 tu,” alisema Sefue.
Ikumbukwe kuwa baada ya kupunguzwa kwa Baraza la Mawaziri kutoka mawaziri 55 wa baraza lililopita hadi mawaziri 34 wa baraza la sasa, hata nafasi za makatibu wa wizara zimepungua pia.
Rais alisema makatibu ambao hawajateuliwa, watapangiwa kazi nyingine.
Kauli ya Dk Mahanga, ambayo aliituma kwenye ukurasa wake wa facebook, iliibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii baada ya wananchi kugawanyika, baadhi wakimuunga mkono na wengine wakimkosoa.
Comments
Post a Comment